Mhusika rasmi katika ‘industry’ ya filamu za Kibongo, Wema Abraham Sepetu (pichani) ametoa kauli iliyojaa mshtuko kuwa, anajipanga kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Akizungumzia na ‘The Five Star Paper’, Risasi Jumamosi ndani ya Hoteli ya The Atriums iliyopo Sinza-Afrikasana, Dar es Salaam juzikati, Wema ambaye ni Miss Tanzania 2006/07 alisema kuwa, katika mipango na ndoto zake za miaka minne ijayo, ni pamoja na kugombea nafasi ya ubunge.

Wema alifunguka kwamba, nyuma ya mpango huo kuna baba yake ambaye aliwahi kutumikia siasa kwa ngazi ya kidiplomasia ikiwa ni pamoja na kuwa balozi ambaye amekuwa akimshauri mara kwa mara kujikita kwenye kilinge cha siasa.

“Mwazo nilikuwa silifikirii sana jambo hilo, lakini baba amekuwa ‘akini-inspire’ mno.
“Nimeshaanza maandalizi kuelekea 2015, naomba Watanzania wanipe sapoti,” alisema Wema.
Alipoulizwa chama na jimbo atakalogombea, Wema alisema:

“Kuhusu chama nitaangalia kitakachokuwa na nguvu hadi kufikia 2014. Jimbo nitakalogombea bado nalitafiti hivyo nitaliweka hadharani ‘leita’.”

Wema ambaye kwa sasa ‘anatoka’ kimapenzi na msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond’ amekuwa akikumbwa na skendo za hapa na pale lakini sasa ameahidi kubadilika ili kujijenga kisiasa.